UMMY MWALIMU:SHULE NI MUHIMU HATA KWA MABINTI WANAOPATA MIMBA UTOTONI
Na:Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema ataendelea kushirikiana na wadau maendeleo ya watoto kuishawishi serikali ili watoto wa kike wanaopata ujauzito warudi shuleni waendelee na masomo.
Ummy aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika maadhimisho ya miaka 70 ya Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF).
“Kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya watoto tunaendelea kuishawishi serikali ili watoto wa kike wanaopata ujauzito warudishwe shuleni waendelee na masomo,” alisema na kuongeza kuwa,
“Nimepata meseji mbalimbali kwenye akanti zangu za Facebook na Twitter watu wananiambia kuwa, watoto wanaobakwa tu ndio warudishwe shuleni. kwa upande wangu mimi naweza kumrudisha shuleni binti yangu akipata ujauzito lakini tuangalie wale wasiyo na uwezo tutakuwa tumepoteza future ya watoto wetu ambao walikuwa na uwezo wa kufanya vizuri darasani,” alisema.
Pia alisema serikali ina mpango wa kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 27 ya mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 13, kupunguza ukatili asilimia 39 mpaka asilimia 20 na kupunguza ukatili wa kingono kwa watoto wakike kutoka asilimia 33 hadi kufikia asilimia 16 na kwa watoto wa kiume kutoka asilimia 14 hadi asilimia saba.
Alisema serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu na kupunguza ukatili wa mabinti kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
Alisema pia lengo la serikali ni kupunguza vitendo vya ukeketaji kwa wanawake kutoka asilimia 15 ya mwaka 2015 hadi kufikia asilimia saba ifikapo 2022.
Kadhalika Ummy alisema kati ya wasichana watatu msichana mmoja amefanyiwa ukatili wa kingono na kati ya watoto wa kiume saba mmoja amefanyiwa vitendo vya ukatili.
Naye Rais Mstaa wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, alisema ni jukumu la kila Mtanzania na Jamii kwa ujumla kushughulikia tatizo la watoto wa mitaani ili kulimaliza.
Alisema watoto wa mitaani wanatakiwa kulelewa majumbani na kupatiwa mahitaji ya kitoto badala ya kulelewa kwenye makambi ambako wanajiandaa kuwa wezi.
Naye Mwakilishi wa UNICEF nchini Maniza Zaman, alisema sekta binafsi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wanaendelea na jitihada za kuhakikisha huduma za watoto zinapatikana kwa maendeleo ya Taifa.

Post a Comment