DABI YA KARIAKOO YAIBUKIA ZANZIBAR KATIKA MICHUANO YA MAPINDUZI
| Mchezaji wa Yanga Donald Ngoma (kulia) akigombea mpira na mlinzi wa kati wa Simba Novalt Lufunga katika moja ya michezo ilizikutanisha timu hizo, ambazo kesho zitachuana huko Zanzibar katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la Mapinduzi. |
Na: Imani Kelvin Mbaga.
Timu za Simba na Yanga zote za jijini Dar er salaam, zinatarajiwa kuumana kesho katika mchezo wa nusu fainali ya pili ya kombe la Mapinduzi, michezo inayoendelea huko visiwani Zanzibar, hiyo ni kutokana na matokeo ya michezo ya mwisho ya kundi A na kundi B iliyochezwa mwishoni mwa juma lililopita.
Yanga inashika nafasi ya pili katika kundi lake baada ya kupokea kichapo cha kushtua cha magoli 4-0 toka kwa viongozi wa kundi hilo ambao ni Azam fc, maarufu kama wana lambalamba, huku Simba wakiongoza kundi lao baada ya kuwatandika Jang'ombe Boys mabao 2-0, katika mchezo uliopigwa siku ya Jumapili jioni.
Kutokana na matokeo hayo, Yanga inayoshika nafasi ya pili, sasa itacheza na Simba inayoshika nafasi ya kwanza katika kundi lake , ukiwa ni mchezo wa nusu fainali ya pili utakaopigwa siku ya Jumanne katika uwanja uwanja wa Amaan Zanzibar majira ya saa 2:15 usiku.
Wapenzi wengi wa soka wangetamani kuziona timu hizi katika mchezo wa fainali, kwa sababu ya mvuto wa mchezo wao ambao nia maarufu kama "Dar es salaam derby", au dabi ya Kariakoo, huku ukivuta hisia ya mashabiki na wapenzi wengi wa soka katika ukanda wote wa Afrika Mashariki.
Mchezo huu unakuja huku timu zote mbili zikiwa zinafukuzana katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara, ambapo Simba wanaongoza ligi hiyo kwa pointi nne zaidi ya wapinzani wao yanga walio katika nafsi ya pili, huku wakiwa pia ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo.
Historia inaonyesha wazi kuwa, timu hizi mbili zinapokutana visiwani Zanzibar, Yanga hawana matokeo mazuri sana mbele ya wapinzani wao, mchezo unaokumbukwa zaidi ni ule wa kombe la Afrika Mashariki na Kati, (hivi sasa Kagame Cup) uliozikutanisha timu hizo katika mchezo wa fainali miaka ya 90' ambapo Simba walishinda mchezo huo kwa njia ya mikwaju ya penalt baada ya kwenda sare kwa dakika 120.
Hata katika michuano ya kombe la Mapinduzi Yanga wamewahi kupoteza kwa magoli 2-0 mbele ya Simba, kitu kinacholeta mvuto wa aina yake katika mchezo wa kesho kuona kama Simba itaendeleza ubabe huko visiwani Zanzibar au la.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza kwenye ligi kuu Tanzania bara, timu hizo ziligawana pointi kwa kufungana goli 1-1, katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam, mchezo ambao ulisababisha vurugu kubwa upande wa mashabiki wa Simba na kuleta uharibifu uliozifanya timu hizo kufungiwa kuutumia uwanja huo kwa muda baada ya vurugu hizo.
Katika mchezo wa kesho, timu zote zinaingia uwanjani huku zikiwa na uwezo na mapunhufu kadhaa kiufundi, ambapo Simba inayojulikana kwa uwezo wao wa kumiliki mpira na kupiga pasi nyingi fupi fupi hasa katikati ya uwanja na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga licha ya kwamba mapingufu yao ni namna wanavyozitumia nafasi hizo.
Yanga wao wamekuja na mfumo mpya ulioletwa na kocha wao kutoka Zambia,George Lwandamina, ambapo ameanza kuutambulisha mchezo ujulikanao kama "total football" ambao huu ndio mchezo alioutumia zaidi akiwa na klabu ya Zesco ya huko nchini Zambia,
Inawezekana mchezo huu utakuwa mgumu hasa kutokana na shinikizo la mashabiki, ukubwa wa mchezo wenyewe, na hata mapungufu ya timu zote yanweza kuufanya mchezo huo kuleta matokeo ambayo hayakutarajiwa na wengi wa wapenda soka.
Kwa ujumla kinachosubiriwa ni mchezo wenyewe ili kuona kile kitakachotokea baada ya dakika 90 za mchezo na kuona ni nani atamtumia mwenzake kama ngazi ya kuelekea fainali ya kombe la Mapinduzi mwaka 2017.
Post a Comment