Your Business Looks Here

Your Business Looks Here
tupo kwenye tathimini ya mwaka radio itarudi hewani kuanzia tarehe 25

MFUMO WA UHIFADHI DATA, NISHATI JADIDIFU KUANZISHWA

 JADI 1
Mtaalam kutoka Sehemu ya Nishati Jadidifu- Idara ya Nishati, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Stephan Kashushura (kushoto) akizungumza na mtaalam  kutoka kampuni ya vifaa vya umeme jua ya Mobisol, Devis Mtete (kulia) mjini Kahama mkoani Shinyanga tarehe 11 Januari, 2017
JADI 2
Mtaalam kutoka kampuni ya vifaa vya umeme jua ya Zola, Omary Raymond (katikati) akielezea shughuli za kampuni yake kwa Mtaalam kutoka Sehemu ya Nishati Jadidifu- Idara ya Nishati, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Stephan Kashushura (kulia). Kushoto ni Msimamizi wa Mradi wa Kuwajengea Uwezo  Wataalam wa Nishati na Tasnia ya Uziduaji  (CADESE) chini ya  Wizara ya Nishati na Madini, Paul Kiwele
…………
Na Mwandishi wetu, Kahama.

Wizara ya Nishati na Madini kupitia Mradi wa Kuwajengea Uwezo  Wataalam wa Nishati na Tasnia ya Uziduaji  (CADESE: Capacity  Development  in the Energy Sector  and Extractive Industries), inatarajia kuanzisha mfumo wa uhifadhi data  kwa ajili ya nishati  jadidifu  ujulikanao kama  Tanzania  Renewable Energy Management  Information System (TREMIS)  utakaowezesha wawekezaji ndani na nje ya nchi  kubaini fursa za uwekezaji zilizopo katika  sekta ya nishati jadidifu.

Hayo yameelezwa na  Msimamizi wa Mradi wa Kuwajengea Uwezo  Wataalam wa Nishati na Tasnia ya Uziduaji  (CADESE), Paul Kiwele katika ziara ya maandalizi ya mfumo huo jana, Kahama mkoani Shinyanga

 Kiwele alisema katika mfumo huo kutawekwa  taarifa mbalimbali kuhusu,  tafiti mbalimbali  na fursa za uwekezaji katika nishati jadidifu , sera, sheria na taratibu ili kuvutia wawekezaji kutoka  ndani na nje ya nchi.

“ Kupitia mfumo huu kutakuwa hakuna haja ya mwekezaji kutoka nje ya nchi kufunga safari  hadi  Tanzania kwa ajili ya kupata  taarifa,  taarifa zote zitakuwepo katika mfumo huu utakaounganishwa na tovuti ya  Wizara ya Nishati na Madini.

Akielezea maandalizi ya mfumo huo, Kiwele alisema kazi ya  maandalizi ya  taarifa kwa ajili kuwekwa kwenye mfumo huo imeshaanza kwa kushirikiana na Kitengo cha Teknolojia  ya Habari na Mawasiliano kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na kuzungumza na wauzaji na waendelezaji wa vifaa vya nishati mbadala katika  wilaya  ya Kahama, Shinyanga kwa ajili ya kupata taarifa zao.

Aliongeza kuwa kutakuwa na warsha itakayokutanisha  wadau mbalimbali wa nishati mbadala ili kupata maoni  yao kuhusu  taarifa zitakazojumuishwa katika mfumo huo.

Mradi wa CADESE unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Maendeleo (UNDP) ulianzishwa mwaka 2014 na unatekelezwa na  Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana n a  wadau wengine kama Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Taasisi ya Uongozi na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF).

No comments

Powered by Blogger.