SIMBA NA AZAM KATIKA MTIFUANO WA MAPINDUZI LEO USIKU
Na. Imani Kelvin Mbaga, Dar es salaam
Timu za
Simba na Azam za jijini Dar es salaam leo zinakutana katika mchezo wa fainali
ya kombe la Mapinduzi, unaotarajiwa kuchezwa visiwani Zanzibar majira ya saa
2:15 usiku katika uwanja wa Aman
Fainali hiyo
inachezwa baada ya Simba kuwaondoa wapinzani wao wa jadi, timu ya Yanga ya
jijini Dar es salaam, katika mchezo wa nusu fainali yapili, kwa njia ya mikwaju
ya penalt 4-2, huku katika nusu fainali ya kwanza Azam waliiondoa Taifa
Jang’ombe kwa goli 1-0.
Mchezo wa
leo unachezwa huku timu zote zikionekana kuwa kwenye kiwango bora hasa
ukizingatia kuwa toka zilipoanza michuano hii hazijawahi kupoteza mchezo
wowote.
Simba
wanaonekana kuwa bora zaidi katika eneo la kiungo wakati mchezaji wao mpya
James Kotei ameoneka kuwa bora kadri sik zinavyozidi kusonga, na kulifanya eneo
la kiungo hasa cha kukaba kuonekana bora kwa klabu hiyo.
Azam
wanaonekana kuwa bora zaidi katika eneo lao la ulinzi hususani ingizo jipya la
Yakub Mohamed anaeonekana kuziba nafasi ya Pazcal Serge Wawa vyema katika eneo
la ulinzi.
Bado timu
zote zinaonekana kupata shida katika namna ya kutengenezana kuzitumia nafasi za
kufunga katika michezo yao licha ya Azam kupata ushindi mnono katika mechi yao
ya mwisho ya makundi dhidi yua timu ya Yanga kwa kuwaadhibu kwa magoli 4-0.
Pamoja na
ushindi huo haiifanyi Azam kuwa bora katika safu yao ya ushambuliaji kwa hiyo
bado kocha msaidizi wa wana lambalamba, Idd Nasor Cheche, ana kazi ya ziada leo
hasa kwa kuwa atakuwa anakutana na safu bora ya ulinzi iliyo chini ya Mzimbabwe
Method Mwanjali.
Kwa upande
wa Simba pia bado washambuliaji wake hawajaonyesha cheche katika michuano yote
na hadi hivi sasa viungo kama Muzamir Yassin na Mohamed Ibrahim “Mo” ndiyo
wanaoonekana kuibeba timu yao katika ufungaji wa magoli jambo ambalo bado ni
hatari kwa mechi kubwa kama ya leo.
Matarajio ya
wachambuzi wengi wa soka ni kuona ufundi mkubwa katikati ya uwanja hasa kwa
baadhi ya wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza na mpira na kuumiliki.
Vita kubwa
kati ya Salum Aboubakar “sure boy”, Frank Domayo “chumvi”, kwa upande wa Azam
na Jonas Mkude na James Kotei kwa upande wa Simba, ambao ndiyo uti wa mgongo wa
kiungo kwa kila upande, bila shaka wao wataamua nini kifanyike na matokeo
yatakuaje.
Baada ya
mechi hiyo timu zote zitarudi Tanzania bara kuendelea na mtifuano wa ligi kuu,
ambako Simba wanaongoza ligi hiyo wakifuatiwa na Yanga katika nafasi ya pili
wakati Azam wanashika nafasi ya tatu.

Post a Comment