BANDARI YAJIPANGA KUPOKEA BOMBA JIPYA LA MAFUTA SAFI
Na Mwandishi wetu,
Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imejipanga kuupokea Mradi wa Bomba Jipya la
Kusafirisha Mafuta Safi kutoka Tanzania hadi Zambia unaotarajiwa kuanza hivi
karibuni.
Mkurugenzi
wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema hayo hivi karibuni
alipokutana na Mawaziri wa Nishati wa Tanzania na Zambia walipofanya ziara ya
kutembelea Boya la Kupokea Mafuta la Single Point Mooring (SPM) ikiwa ni hatua
ya kukamilisha ziara yao ya kutembelea njia ya Bomba la TAZAMA na Vituo vya
Kusukuma Mafuta waliyoianza jijini Ndola, Zambia na kumalizikia jijini Dar es
Salaam, Tanzania.
Aliyasema
hayo kufuatia wito wa Waziri wa Nishati wa Zambia, Mulumba David alipoikumbusha
Mamlaka hiyo kuhusiana na kauli iliyotolewa na Rais wa Zambia, Mhe. Edgar Lungu
wakati alipofanya ziara nchini mwezi Novemba Mwaka jana na kuitaka kuhakikisha
inaongeza ufanisi wa utoaji huduma zake ikiwemo kuboresha Teknolojia ya kupokelea
mafuta.
Mhandisi
Kakoko alisema anakumbuka vyema kauli hiyo ya Rais Lungu na aliongeza kwamba
Mamlaka ya Bandari imejipanga vizuri kuhakikisha inatoa huduma zenye kiwango na
kwamba hawapo tayari kupoteza ushirikiano wa kibiashara na Zambia.
“Mlimsikia
Rais Lungu alisema wazi Wazambia na Watanzania ni ndugu wa damu lakini alionya
kwamba biashara inaweza isiwe ndugu kama tunaichezea; na akasema ni vizuri tuwe
na ufanisi na tuwe na gharama ndogo ili Wazambia waweze kufaidi vinginevyo
atakwenda kwingine; jambo hili hatuwezi kuruhusu litokee,” alisema Mhandisi
Kakoko.
Alibainisha
kuwa, Mamlaka hiyo inapitia upya gharama zake kwa Zambia hususan ikizingatiwa
kuwa hivi sasa kuna ushindani mkubwa hasa baada ya Msumbiji kuwa eneo salama.
Aliongeza
kuwa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 wamejipanga vyema kufanya maandalizi yote ya
kuimarisha na kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka hiyo kwenye suala la ushushaji
wa mafuta ikiwemo kuweka Gati litakalohudumia Meli nyingi zaidi na kwa haraka
zaidi. “Tunajipanga ili Bomba hili jipya likikamilika liweze kuunga moja kwa
moja,” alisema.
Katika
ziara hiyo, ilielezwa kwamba Serikali za Tanzania na Zambia zimefanya tathmni
ya kuanza utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Bomba jipya la Mafuta Safi na
kwamba taratibu mbalimbali zimeanza kutekelezwa.
Post a Comment