MAWAZIRI UGANDA NA TANZANIA WATEMBELEA ENEO LITAKAPOJENGWA GATI ITAKAYOTUMIKA KUPAKIA MAFUTA KUTOKA UGANDA KWENYE MELI
Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Mhandisi Irene Muloni wametembelea eneo la Chongoleani mkoani Tanga ambako kutajengwa hifadhi ya mafuta pamoja na gati itakayotumika kupakia mafuta kwenye Meli mbalimbali ili kusafirishwa.
Mafuta hayo yatapakiwa kwenye Meli hizo baada ya kusafirishwa na Bomba kutoka Hoima nchini Uganda kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.
Akiwa katika eneo hilo Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda aliwaeleza wananchi wa eneo hilo kuwa nchi ya Uganda inaishukuru Tanzania kwa kukubali Bomba hilo lipite katika ardhi ya Tanzania suala ambalo litakuwa na faida mbalimbali kwa Wananchi ikiwemo mabadiliko ya kiuchumi.
Alisema kuwa lengo ni kuona kuwa mradi huwa huo unaanza kazi mwaka 2020 na ndiyo maagizo ambayo Marais wa nchi mbili wameyatoa kwa watendaji wanaosimamia Mradi huo wa Bomba la Mafuta.
Mhandisi Muloni alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kujiandaa kikamilifu kwa fursa za kiuchumi kwani watekelezaji wa mradi watahitaji huduma mbalimbali kama za chakula, malazi na usafiri hivyo kupitia utoaji wa huduma hizo wananchi nao watapata kipato.
Pia alizishukuru Sekta Binafsi za Uganda na Tanzania kwa kuwa tayari kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa akitolea mfano kampuni ya GBP ya Tanzania ambayo imeonesha nia ya kununua hisa katika kampuni itakayoanzishwa kwa ajili ya usimamizi wa Bomba hilo la Mafuta.
Post a Comment