SERIKALI YASITISHA MCHAKATO WA MABADILIKO SIMBA NA YANGA
Katibu mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja |
Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT),
imesitisha michakato yote ya ubadilishaji wa umiliki wa vilabu vya wanachama
hususani Simba na Yanga ambavyo kwa siku za karibuni vimekuwa kwenye mchakato
wa kubadilisha umiliki kwa Simba kujiendesha kwa mfumo wa hisa na Yanga
kujiendesha kwa mfumo wa kukodishwa.
Akitoa taarifa
hiyo mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, katibu mkuu wa BMT,
Mohamed Kiganja alisema hadi hivi sasa kumekuwa na malalamiko mengi juu ya
michakato hiyo kutoka kwa baadhi ya wanachama hadi kufikia hatua ya kupelekana
mahakamani kitu ambacho ni hatari kwa amani ya taifa letu.
Kwa mujibu wa
taarifa rasmi ya serikali iliyosomwa mbele ya waandishi wa habari na katibu
mkuu huyo, marufuku hiyo inaendana na agizo kwa vilabu kufanya marekebisho ya
katiba zao kwa mujibu wa sheria ya Baraza la Michezo la Taifa na kanuni za
msajili Namba 442 Kanuni ya 11 Kifungu kidogo cha (1-9)
Baraza limesema
linapenda kuona wahusika wanafuata sheria za nchi katika kutimiza malengo yao
na kwamba kuendelea na mchakato huo bila kufuata utaratibu na kufuata sheria za
nchi ni kosa na hatua stahiki zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo
hayo.
Baada ya hatua
ya kutoa tamko la usitishwaji huo Baraza la Michezo la Taifa litapeleka barua
kulitaarifu shirikisho la soka nchini (TFF) kuhusu agizo hilo kwa wanachama
wao.
Klabu ya Simba
tayri ilikuwa inaendelea na mchakato wa kuandaa mazingira ya kuuza hisa ili
klabu hiyo imilikiwe na Mohamed Dewj “Mo” kwa asilimia 51 ya hiosa huku wana hisa
wengine wakimiliki kwa asilimia 49, wakati Yanga walikuwa na mchaskato wa
kukodisha klabu yao kwa kampuni ya Yanga Ltd inayomilikiwa na mwenyekiti wa
klabu hiyo Yusuph Manji.
Kwa nyakati
tofauti viongozi wa vilabu hivyo walisema hawawezi kusema chochote chochote
hadi hapo watakapopata barua rasmi juu ya tamko hilo.
Katibu mkuu wa BMT (aliyevaa tai) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam |
Post a Comment