SERENGETI BOYS KUPAA KESHO KUELEKEA KOREA
Kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya serengeti boys |
Kikosi cha timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 Serengeti boys cha wachezaji 19 na viongozi 6 kinatarajia kuondoka nchini kesho saa 10:30 jioni kwa ndege ya shirika la ndege la Emirates kuelekea Korea ya kusini kwa michezo ya kimataifa ya kirafiki kwa mwaliko wa shirikisho hilo.
Kwa mujibu wa habari zilizotolewa na shirikisho la soka la Tanzania, TFF, zinasema kuwa kikosi hicho kitasafiri hadi Dubai kabla ya kubadilisha ndege kuelekea Korea Kusini.
Wachezaji wanaotarajia kusafiri hiyo kesho ni pamoja na Muhsin Makame, Ramadhani Gadafi, Shaaban Zubeir Ada, Mohamed Abdallah Rashid, Dickson Joff, Kibwana Ally Shomari, Asad Juma, Cyprian Mutesigwa, Ramdhan Kabwili, Nashon Kelvin, Ally Msengi, Kelvin Kayego, Samweli Blazio, Nikson Kibabage, Israel Mwenda, Henrick Vitalis, Ally Ng'anzi na Issa Makamba wakiwa na kocha wao Bakari Shime Nyundo "mchawi mweusi" , msaidizi wake Muharami Mohamedi, daktari wa timu Sheick Mgazija, mtunza vifaa ni Edward Venance, mshauri wa soka la vijana wa TFF Kim Polsen na mkuu wa msafara huo atakuwa ni mkurugenzi wa ufundi wa TFF Salumu Madadi.
Timu hiyo ilitolewa kwenye mashindano kufuzu michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 itakayofanyika Madagascar mwakani kwa kupoteza mchezo wa marudiano dhidi ya Congo Brazzaville kwa goli 1-0 na kufifisha matumaini ya Watanzania kuiona timu hiyo ikishiriki fainali za vijana licha ya kwamba TFF imekata rufaa dhidi ya mchezaji mmoja wa Congo anayetuhumiwa kuwa na umri usiostahili.
Korea ya Kusini imeandaa michuano ya mataifa sita ikiwemo Tanzania itakayoanza mwishoni mwa juma kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 na kutoa fursa kwa vijana wa Tanzania kupata uzoefu wa mashindano ya kimataifa kabla ya kuanza michuano mingine inayowahusu vijana barani Afrika, huku shirikisho la soka nchini Tanzania likiipandisha hadhi timu hiyo kuwa timu ya taifga ya vijana chini ya miaka 20 yaani Ngorongoro Heroes.
Post a Comment