IDD CHECHE USO KWA USO NA KOCHA BORA AFRIKA, AZAM WAKIIVAA MAMELODI
Jafar Idd Maganga, msemaji wa klabu ya Azam fc |
Na: Imani Kelvin Mbaga, Dar es salaam
Klabu ya Azam fc ya jijini Dar es salaam, imethibitisha kukubali kucheza na mabingwa wa ligi ya mabingwa barani Afrika, timu ya Mamelodi Sundowns kutoka Afrika ya Kusini, ambao wapo nchini kwa kambi ya siku nne kujiandaa na ligi ya nchini kwao lakini pia wakijiandaa na mechi yao na TP Mazembe katika mchezo unaoashiria kuuanza msimu mpya wa michuano ya vilabu barani Afrika.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, msemaji wa wana lambalamba, Jafar Idd Maganga, alisema kuwa licha ya michezo ya ligi inayoendelea hivi sasa huku wakiwa na mchezo mgumu dhidi ya Ndanda ya Mtwara siku ya Jumamosi, lakini wamekubali kucheza na Mamelodi kwakuwa ni timu kubwa barani Afrika na kwao itakuwa ni mechi muhimu ili kujipima ngumu.
Maganga alisema hiyo itakuwa ni mechi nyingine ambayo kocha mzawa anaekiongoza kikosi hicho kwa sasa Idd Nasor Cheche, atapata nafasi ya kuonyesha uwezo wake katika anga za kimataifa, baada ya kujitengenezea jina kubwa kwa kuvifunga vigogo vya soka nchini, Simba na Yanga katika yakati tofauti.
Awali taarifa zilizopatikana ni kuwa mabingwa hao wa Afrika wangecheza na vigogo wa soka hapa nchini kabla ya timu hizo, Simba na Yanga kukataa kucheza michezo yao na timu hiyo kwa madai ya kubanwa na ratiba ya ligi, ambapo Simba wanatarajia kusafiri kuelekea mkoani Ruvuma kucheza na Majimaji ya huko wakati ambapo Yanga wanatarajia kubaki jijini Dar es salaam kuwakaribisha Stand United
Post a Comment